MANCHESTER UNITED YAMFUTA KAZI MENEJA WAO

Jose Mourinho amefutwa kazi wadhifa wake kama meneja wa Manchester United.
Klabu hiyo imetangaza kwamba ameondoka katika klabu hiyo mara moja.
"Klabu hii ingependa kumshukuru Jose kwa kazi yake kipindi ambacho amekuwepo Manchester United na inamtakia kila la heri siku za usoni."
Meneja mpya wa muda atateuliwa kuongoza klabu hiyo hadi mwisho wa msimu, huku klabu hiyo ikiendelea na mchakato wa kumtafuta meneja mpya wa kudumu."
Mourinho, 55, amekuwa Old Trafford kwa miaka miwili unusu pekee, baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Mholanzi Louis van Gaal mwezi Mei mwaka 2016.
Mreno huyo alikuwa ametia saini kandarasi mpya mnamo mwezi Januari ambayo iliimarisha mafao na mahitaji yake ya kikazi mbali na kumuongezea kandarasi yake hadi mwaka 2020.
Alishinda Kombe la Ligi na Europa League akiwa Manchester United lakini kwa sasa wamo alama 19 nyuma ya viongozi wa Ligi Kuu ya England kwa sasa, ambao ni Liverpool waliowachapa 3-1 Jumapili.
Hali ya United kwa sasa, ambapo wamezoa alama 26 pekee baada ya kucheza mechi 17 za msimu Ligi ya Premia ndiyo mbaya zaidi katika historia ya klabu hiyo hatua kama ya sasa tangu msimu wa 1990-91.

Wamo alama 11 nyuma ya klabu nne za kwanza kwenye jedwali, ambazo hufuzu kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Wanakaribia zaidi eneo la kushushwa daraja kuliko kileleni.
Yamkini mwezi Desemba si wa bahati kwa Mreno huyo, alifutwa kazi tarehe 17 Desemba mwaka 2015 na klabu ya Chelsea baada ya klabu hiyo kuandikisha msururu wa matokeo mabaya.
The Blues walikuwa wameshinda Ligi ya Premia msimu uliotangulia lakini msimu huo mambo yakawaendea kinyume, na walikuwa alama moja tu juu ya eneo la kushushwa daraja ligini.
No comments:
Post a Comment